BARA BARA YAPEWA JINA LA KIKWETE HUKO KENYA
Serikali ya kaunti ya Nairobi nchini
Kenya imebadilisha jina la barabara moja na kuipa jina la Rais wa
Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.
Kiongozi huyo alikuwa nchini Kenya
kwa ziara ya siku tatu na Jumanne alihutubia kikao cha pamoja cha Bunge
la Seneti na Bunge la Kitaifa.
Rais Kikwete alihudhuria sherehe ya kubadilisha jina barabara hiyo ya Milimani iliyoko karibu na ikulu ya Nairobi.
Barabara
hiyo yenye urefu wa kilomita 0.49 huanzia makutano ya barabara ya
Kenyatta Avenue na Valley Road na kufululiza hadi barabara ya Dennis
Pritt.
"Rais Kenyatta aliposema kwamba utazuru hapa tulishauriana
kujua iwapo tungeweza kubadilisha jina la barabara hii na kwa kuwa sisi
ni marafiki, alikubali, na kama uonavyo, inaelekea hadi lango la ikulu
yake (Bw Kenyatta),” Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero alimwambia Bw
Kikwete, kwa mujibu wa gazeti la The Star la Kenya.
Barabara hiyo imo karibu na barabara ya Nyerere.
Rais
Kikwete sasa anajiunga na kiongozi wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere
na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume katika kuwa na
barabara zilizopewa majina yao Nairobi.
Kabla ya kuondoka
mamlakani mwaka 2013, aliyekuwa rais wa Kenya wakati huo Mwai Kibaki,
alibahatika kuwa na barabara yenye jina lake jijini Dar es Salaam.
Sherehe
ya kubadilisha jina la barabara hiyo ya Old Bagamoyo ilihudhuriwa na Bw
Kibaki mwenyewe, Rais Kikwete na Bw John Magufuli aliyekuwa waziri.
Bw Magufuli kwa sasa ni mgombea wa urais wa chama tawala cha CCM.
Comments
Post a Comment