Mwanamke mwenye 'macho ya ajabu akamatwa

Sharbat Gula baada ya kufikishwa kortini Peshawar Oktoba 26, 2016


Mhamiaji kutoka Afghanistan, ambaye alipata umaarufu picha yake ilipochapishwa kwenye ukurasa wa kwanza wa jarida la National Geographic miaka thelathini iliyopita, amekamatwa.

Maafisa wanasema amekamatwa kwa kuwa na nyaraka bandia za utambulisho.
Sharbat Gula alipata umaarufu mwaka 1985 kutokana na picha hiy aliyopigwa akiwa na umri wa miaka 12.
Macho yake yalikuwa na rangi ya kijani, jambo lililomfanya kufahamika kwa jina 'Green-eyed Girl'.
Maafisa wanasema alikamatwa na Idara ya Uchunguzi ya Pakistan (FIA) baada ya uchunguzi wa miaka miwili Peshawar, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan.
Pakistan ilianza kuwasaka watu wenye vitambulisho bandia majuzi.
Bi Gula aliwasilisha ombi la kutaka kitambulisho Aprili 2014 akitumia jina Sharbat Bibi.
Iwapo madai hayo yatathibitishwa, basi atakuwa mmoja wa maelfu ya wakimbizi kutoka Afghanistan ambao wamejaribu kukwepa mfumo wa usajili wa watu unaotumia kompyuta nchini Pakistan.
Afisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usajili wa Watu (Nadra) amesema maafisa wa FIA pia wanawatafuta wafanyakazi watatu ambao wanadaiwa kumpa kitambulisho Bi Gula.
Gazeti la Dawn la Pakistan limesema Bi Gula alipewa vitambulisho pamoja na wanaume wengine wawili waliodai kuwa wanawe wa kime.
Sharbat Gula baada ya kufikishwa kortini Peshawar Oktoba 26, 2016
Picha maarufu ya Bi Gula ilipigwa 1984 alipokuwa kambi ya wakimbizi kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Wakati huo wanajeshi wa Muungano wa Usovieti walikuwa wameingia Afghanistan.
Mwaka 2002, mpiga picha Steve McCurry alimtafuta na kumpiga picha. Wakati huo alikuwa anaishi kijiji kimoja Afghanistan akiwa na mumewe na binti zao watatu.
Baada ya kutokea kwa habari za kukamatwa kwa Bi Gula, Bw McCurry amesema atafanya kila juhudi kumsaidia kifedha na kisheria.
"Nimejitolea kufanya kila niwezalo kutoa msaada wa kifedha na kisheria kwake na familia yake," aliandika kwenye Instagram.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha Pakistan inatoa hifadhi kwa wakimbizi 1.4 milioni kutoka Afghanistan ambao wamesajiliwa. Inakadiriwa kwamba wengine milioni moja wanaishi humo lakini hawajasajiliwa.

Comments