Wachina mbaroni kwa utekaji

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia raia wawili wa China kwa tuhuma za kumteka nyara Mchina mwenzao, Liu Hong (48) ambaye ni mfanyakazi wa Le Grande Cassino, wakidai kulipwa Dola za Marekani 19,000 (zaidi ya Sh milioni 38).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema walipokea taarifa kwamba raia huyo wa China alitekwa nyara na watu wasiofahamika.
Alisema taarifa hizo zilieleza kwamba Liu alitekwa nyara Oktoba 23, mwaka huu saa moja asubuhi na ndipo polisi wakaunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini watekaji walikuwa wakidai Yen 100,000 (fedha za China) ambazo ni sawa na Dola za Marekani 19,000.
“Oktoba 24, mwaka huu saa 11 jioni kikosi kazi cha wizi wa makosa ya kimtandao cha Polisi Kanda Maalumu walibaini kuwa wateka nyara hao wapo katika Hoteli ya Palm Beach Upanga na walipofika hapo wakaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema polisi walipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua mlango ndipo polisi waligundua wateka nyara hao kuwepo katika chumba hicho.
Alisema wakiwa wanajiandaa kuvunja mlango, mara mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing (37) raia wa China aliamua kufungua mlango na kumkamata akiwa na Liu ambaye ni mtekwa nyara.

Comments