FANJA FC YA OMANI YAMSHIKA PABAYA NGASA NA MBEYA CITY YAKE


Pamoja na kumalizana na Mbeya City, bado hakijaeleweka kwa kiungo mshambuliaji, Mrisho Ngassa ambaye juzi Jumamosi alilazimika kukaa jukwaani kushuhudia timu yake mpya ikigawana pointi na timu yake ya zamani, Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Ngassa amesaini mwaka mmoja Mbeya City, lakini juzi alishindwa kuitumikia kutokana na kutokuwa na Kibali cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC), ambacho kimechelewa kufika kutokana na timu alikotoka, Fanja ya Oman kutokitoa kwa wakati.

Kocha wa timu hiyo, Kinnah Phiri, amesema, mbali na Ngassa pia alishindwa kumtumia straika Zahoro Pazzi kwa tatizo kama hilo kutoka katika timu ya FC Lupopo ya DR Congo, lakini kufikia mchezo ujao dhidi ya Toto Africans, tatizo hilo litakuwa limetatuliwa.

Aidha, Phiri amelizwa na kitendo hicho kwa kile alichoamini kwa nafasi walizozitengeneza, kwa vyovyote vile Ngassa asingekosa mabao kuanzia mawili.

“Tuliwachezea nusu uwanja, tulitengeneza nafasi zaidi ya 10, lakini ajabu mechi ikaisha bila-bila, inauma na ninaamini kama Ngassa angekuwemo asingekosa mabao mawili, japo lazima nikubali (Juma) Kaseja alikuwa msaada mkubwa kwa wenzetu.

“Alitoa hatari nyingi mpaka kuwafanya washambuliaji wetu kukata tamaa lakini tunajipanga na mechi zinazofuatia,” alisema Mmalawi huyo.

SOURCE: CHAMPIONI

Comments