MAAFISA WAWILI WA TRA KUPANDA KIZIMBANI KESHO
TRA |
Kesi ya kuomba na kupokea rushwa inayowakabili maofisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itatajwa kesho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Washtakiwa wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kuomba na kupokea rushwa ni Liberatus Rugumisa (30) na Keneth Mawere (29), ambao ni maofisa wasaidizi wa kodi kutoka TRA. Mshtakiwa mwingine ni Nassoro Nassoro (42) ambaye siyo mtumishi wa mamlaka hiyo.
Washtakiwa ambao wote ni wakazi wa Kigamboni walifikishwa mahakamani hapo Desemba 13 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Adolf Sachore.
Wakili kutoka Takukuru, Lupyana Mwakatobe alidai Rugumisa na Mawere katika shtaka la kwanza, Novemba 18, katika ofisi za TRA zilizopo Kariakoo waliomba rushwa ya Sh50 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Humphrey Lema ili wampunguzie kodi aweze kulipa kiasi kidogo cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati wakijua ni kinyume na sheria.
Katika shtaka la pili linalowakabili maofisa hao wa TRA, Mwakatobe alidai Novemba 23, kwenye duka la kubadilishia fedha za kigeni la Cate lililopo Kariakoo, mitaa ya Nyamwezi na Donge, walijipatia Sh10 milioni kutoka kwa Lema ili wampunguzie kodi, aweze kulipa kiwango kidogo cha VAT.
Mwakatobe alidai shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote, ambao Desemba Mosi, katika ofisi za TRA zilizopo Kariakoo, wanadaiwa kwa njia ya ushawishi, walipokea rushwa ya Dola 2,744 za Marekani kutoka kwa mfanyabiashara huyo, wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Comments
Post a Comment