MANISPAA YA SONGEA INA ZIADA YA MADAWATI 597



Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imefanikiwa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekaa chini baada ya kuwa na ziada ya madawati 597.
Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema Manispaa  hiyo yenye shule za msingi za serikali 76 ina wanafunzi 47,314 ambao wanahitaji madawati 15,771.
Amesema madawati yaliokuwepo kabla ya agizo la Rais ni 9,759,madawati yaliotengenezwa baada ya agizo la Rais ni 6,609 ambapo hadi sasa madawati yaliotengenezwa ni 16,368 hivyo kuwa na ziada ya madawati 597.
 “Halmashauri imefanikiwa kufikia lengo hilo kwa kuwa na madawati 16,368 kati ya Madawati 15,771 yaliyohitajika  hadi sasa hakuna Mwanafunzi anayekaa chini.Jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa tatizo hilo halijirudii kwa kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa na kukarabatiwa pale inapotakiwa kufanya hivyo’’,anasisitiza Midelo.
Hata hivyo amesema,ziada ya madawati imetokana na Halmashauri kupata msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ikiwemo msaada toka Ofisi ya Bunge madawati 537,kampuni ya Matra madawati 50,Wakala wa misitu madawati 70 na wadau wengine.
Kuhusu utengenezaji wa meza na viti katika shule 24 za sekondari za serikali katika Manispaa hiyo,Afisa habari huyo amesema kuna jumla ya meza 852 na viti 852 ambavyo  vimetengenezwa hivyo kumaliza tatizo la upungufu wa meza na viti katika shule za sekondari.
Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa ametoa agizo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi nchini ambao bado hawajakamilisha utengenezaji wa madawati kuhakikisha hadi Desemba 30 mwaka huu madawati yawe yamekamilika.

Comments