MZEE WA UPAKO KUANZA KUUZA GONGO MWAKANI
Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee
wa Upako jana amesema waandishi wote wa habari wanaoandika habari za
kumchafua, watakufa kabla ya kufika Machi 2017.
Kauli
hiyo ameitoa ikiwa ni mwendelezo wa mahubiri yake ya nne katika wiki ya
tatu mfululizo, akijibu yale yaliyoandikwa katika vyombo vya habari
kuhusu kumfanyia fujo jirani yake na kulewa.
“Kila
mwandishi aliyeniandika vibaya, ikifika mwezi wa tatu akiwa hai, mimi
naacha kuhubiri, nafunga virago nakwenda kuuza gongo, sasa Mungu ndiye
ataamua kwamba ama niache kuhubiri mimi au wewe ufe …najua hata leo mko
humu mmekuja na mnasikiliza tu,” alisema.
“Akisema
Mungu uishi wewe basi, nakuwa sina namna, lakini sijawahi kumtumikia
Mungu ambaye ananyamaza. Nilishakubaliana mimi na Mungu, mpango wa Mungu
ndiyo mpango wangu, sasa wajiandae, mimi siyo Sheikh Yahaya, mmeingia
choo cha kike, nasema ‘Mama yangu mzazi’ nitaacha kuhubiri, nitaacha
kuhubiri ….mimi nina nguvu saaana,”alisema.
Hata hivyo baadaye mchungaji huo alishuka na kusema anamuachia Mungu wake ambaye atawahukumu kwa wakati wake.
“Lakini Mungu anasema tusihukumu, namuachia Mungu atawahukumu kwa wakati wake, haleluya, haleluya, Mungu awabariki sana."
Novemba
24, mitandao ya kijamii ilikuwa na picha zinazomuonyesha Mzee wa Upako
akirushiana maneno makali na jirani huyo ambaye anasikika sauti.
Taarifa
za kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kiroho zilisambaa baada ya mwandishi
wa habari, Happiness Katabazi aliyeshuhudia tukio hilo, kuandika kwa
urefu kisa hicho na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Novemba
26, Mzee wa Upako kwa mara ya kwanza alisita kuzungumzia sakata hilo na
badala yake akasema wanaomtuhumu waendelee kusema: “Sisemi, lakini
siogopi kwenda jela mimi na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini
hawatashinda. Hii ni kama kumpiga chura teke.”
Novemba
28, pia Mchungaji huyo akajibu akisema maneno aliyotumia ambayo ni
mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo matusi kwani yameandikwa kwenye biblia
na kwamba watu hao ndiyo walianza kumtukana yeye baada ya kuwauliza
wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Jana,
mchungaji huyo aliwahakikishia waumini wake akisema waandishi
walioandika kwa lengo la kumchafua watakufa kabla ya kufika Machi
mwakani.
Katika
mahubiri yake yaliyojengwa na msingi wa Biblia kutoka kitabu cha
Samweli wa kwanza, sura ya 16, mstari wa saba, Mzee wa Upako
aliyekaribishwa kwa nyimbo kadhaa ikiwamo ‘kusanya kusanya’ alisema yeye
siyo mchungaji anayejikweza, lakini baadhi ya wachungaji wakubwa kutoka
nje wamekuwa wakienda kuomba upako.
Pia, alisema hata Rais John Magufuli hakumuita yeye bali aliona kitu ndani yake na kubarikiwa kabla ya kumtembelea.
Comments
Post a Comment