NYAYO ZA BINADAMU WA KALE ZAONEKANA TANZANIA
Alama za Nyayo Za Kale |
Nyayo zilizoachwa na binadamu wa
kale mamilioni ya miaka iliyopita zimegunduliwa nchini Tanzania karibu
na pahala ambapo nyayo sawa na hizo ziligunduliwa miaka ya 1970.
Alama hizo za miguu ziliachwa na binadamu wa kale walipotembea kwenye matope na majivu ya volkano yaliyokuwa hayajakauka.Wataalamu wanakadiria kwamba viumbe ambao hujulikana kama Australopithecus afarensis, ndio walioacha nyayo hizo, na walikuwa na kimo na unene uliotofautiana.
Wanasayansi wanasema nyayo hizo zinaashiria jinsi binadamu wa kale walivyoishi.
Australopithecus afarensis ni miongoni mwa aina ya binadamu wa kale wanaofahamika zaidi na ambao waliishi kipindi kirefu.
Visukuku vya "Lucy", mwanamke kijana aliyeishi Ethiopia zaidi ya miaka 3.2 milioni, ndiye maarufu zaidi kutoka kwa kundi hilo la binadamu.
Nyayo hizo zilizogunduliwa huenda ziliachwa na mwanamume aliyekuwa labda anatembea na wenzake wa kike wadogo kwa kimo.
"Ushahidi huu mpya, ukiuzingatia pamoja na ushahidi wa awali, unaashiria kwamba binadamu wa kale walikuwa wanatembea kama kundi kwenye mandhari ambapo kulikuwa na matope, majivu na mawe ya volkano baada ya kulipuka kwa volkano na mvua kunyesha. Lakini kuna zaidi," amesema mtafiti mkuu Prof Giorgio Manzi, mkurugenzi wa mradi huo wa akiolojia nchini Tanzania.
"Nyayo za mmoja wa binadamu kati ya zile tulizogundua ni kubwa kuliko za wengine katika kundi hilo, jambo linaloashiria kwamba huenda alikuwa mwanamume.
"Kusema kweli, kimo cha 165cm ambacho kinadokezwa na nyayo hizo kinamfanya kuwa moja wa binadamu wa Australopithecus warefu zaidi kugunduliwa hadi wa leo."
Comments
Post a Comment