ONESHO LANGU LA UJERUMANI LIMEFANIKIWA

Msanii Ben Paul
Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ben Paul amefurahishwa na mafanikio aliyoyapata katika onesho lake alilolifanya Offenbach, Ujerumani, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julisu Nyerere akitokea Ujerumani jana, Paul alisema amepata mafanikio makubwa katika onesho hilo kwani amepata mashabiki ambao hakuwatarajia. Alisema hayo ni mafanikio makubwa kwake hasa kwa vile aliimba ‘live’ katika nchi iliyo nje ya Afrika.
“Onesho langu la Ujerumani limefanikiwa sana na nimeona kuna mwanga mbele yangu, mashabiki wangu wajue hilo,” alisema kwa furaha mtaalamu huyo wa wimbo wa Moyo Mashine.
Alisema katika onesho hilo Mwafrika alikuwa peke yake na akitumbuiza ‘live’ wimbo wake wa Moyo Mashine, Wajerumani walionekana kuufurahia.
Alisema watu takriban 10,000 walihudhuria onesho hilo na limeacha historia katika maisha yake.
“Katika maisha yangu onesho lile ni la tatu kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki, ikiwa ni pamoja na onesho la Fiesta lililofanyika Dodoma kwa wabunge wengi kupanda jukwanii na onesho lingine lilikuwa usiku wa Mwafrika ambalo nalo lilikuwa na watu wengi,” alisema.

Comments