POLISI WASHINDWA TENA KUMFIKISHA MAHAKAMANI BOSI WA JAMII FORUM
Mwanzilishi wa Jamii Forums Maxence Melo |
Polisi jijini Dar es Salaam, kwa siku nyingine wamesindwa kumpeleka mahakamani Maxence Melo,
ambaye ni mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums.
Taarifa kutoka kwa Jamii Forums inasema Bw Melo alizuiliwa kwa kutotoa taarifa za watumiaji wa mtandao huo.Alitarajiwa kufikishwa kortini Jumatano lakini hilo halikufanyika.
Badala yake, polisi walifika afisi za Jamii Forums kufanya upekuzi kisha wakawahoji wafanyakazi na kuchukua maelezo ya utendaji kazi wao.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanasema Melo anashikiliwa kinyume cha sheria kwani sheria inataka mtu asishikiliwe na polisi kwa muda unaozidi saa 24 bila kuwasilishwa kortini.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa taarifa Jumatano kulaani kuendelea kuwekwa kizuizini kwa Bw Melo.
"Kituo kinalitaka jeshi la polisi kuheshimu katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 1977 inayotoa haki kwa kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru," taarifa ya kituo hicho ilisema.
Kupitia taarifa, mratibu wa kitaifa wa shirika la watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania (THRDC) Bw Onesmo Olengurumwa aliwataka maafisa wa polisi kumwachilia huru mara moja Bw Melo kwa sababu "wameshindwa kumfungulia mashtaka kortini katika muda unaotakikana kisheria."
Aliitaka serikali kuhakikisha Sheria ya Makosa ya Kimtandao haitumiwi kukandamiza uhuru wa kujieleza katika mtandao nchini Tanzania.
Wakili wa Melo, Jebra Kambole anasema Ijumaa wana mpango wa kuiandikia Mahakama Kuu ombi la kuiomba iwalazimishe polisi kumpeleka Melo mahakamani hapo afunguliwe mashtaka au aachiliwe
Comments
Post a Comment