SIRI YA TAULO LA IVO MAPUNDA HII HAPA

Aliyekuwa golikipa a vilabu mbalimbali vikubwa Afrika Mashariki ikiwemo Simba, Yanga, Azam, Gor Mahia na Taifa Stars, Ivo Mapunda amefichua siri ya taulo lake alilokuwa akilitumia wakati akiidakia Simba na kusema kuwa taulo lile lilikuwa na siri kubwa.

Ivo amesema taulo lile halikuwa na kitu chochote cha kishirikina, isipokuwa aliamua kucheza na saikolojia ya wachezaji hususani wa Yanga ili kuwavuruga na kuwatoa mchezoni.

Amesema lilikuwa ni jambo la kushangaza kuona wachezaji wanashindwa kufunga kwa uwezo wao na badala yake wanapeleka hisia zao kwenye taulo ambalo halihusiki kabisa na mchezo, na ndiyo maana aliamua kufanya makusudi ili kuwatoa mchezoni.

"Nilikuwa nacheza na akili zao, na saikolojia yao, nilipogundua wanaogopa taulo nikaamua niling'ang'aie makusudi ili kuwatoa mchezoni, lakini lilikuwa halina jambo lolote la kishirikina zaidi ya kunisaidia kufuta jasho" Amesema Ivo.

Baadhi ya wachezaji hasa wa yanga katika mchezo kati yao na Simba walikuwa wakilitilia shaka taulo hilo kwa kudai kuwa ndilo sababu ya wao kutopata mabao, kiasi cha kulalamika kwa mwamuzi kuwa taulo lile lilikuwa halipaswi kukaa katika nyavu za goli.

Katika hatua nyingine, golikipa huyo mkongwe ambaye amestaafu, ameamua kuanzisha kituo cha michezo kwa ajili ya vijana na sasa yuko katika hatua za kati za kutafuta wadau, ambapo amepanga kuanza na mchezo wa soka, na baadaye kitakuwa kikihusika na michezo yote.

Comments