WALIMU, MADAWATI CHANGAMOTO ELIMU BURE

Na Samwel Andrew, Dodoma


Changamoto ya utolewaji wa elimu bora kwa baadhi ya maeneo imeendelea kujitokeza kwa namna tofauti, mbali ya serikali kuendelea na msimamo wake wa kuwa inatoa elimu bora kwa shule zake.
Upatikanaji wa madawati kwa shule hizo sio sababu ya kueleza moja kwa moja kuwa elimu wanayopata watoto ni bora na inakidhi viwango vinavyotakiwa, huku baadhi ya shule mkoani hapa zikiwa bado na tatizo la ukosefu wa madawati.
Sospeter Nhonya Mazengo, ni Diwani wa kata ya Chahwa, Manispaa ya Dodoma, ameeleza changamoto zinazoikabili shule ya msingi Chahwa, hususani upungufu wa madarasa katika wakati huu wa elimu bure.
Mbali ya changamoto hiyo ya upungufu wa madarasa, shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi kukosa sehemu ya kujistiri kwa muda mrefu sasa.
Aidha, suala la vitisho kwa walimu kutoka kwa wazazi nayo ni moja ya mambo yanayopelekea shule hiyo kutokuwa na taaluma bora kwa watoto wanaosoma shuleni hapo, huku ikielezwa kuwa ni mfumo wa maisha wanayoishi wakazi wa eneo hilo.
Shule ya msingi Chahwa, inakabiliwa na upungufu wa walimu kulingana na wanafunzi waliopo, ambapo ina jumla ya walimu 6, ikiwa na upungufu wa walimu 6 ili kuwa 12 wanaohitajika kwa idadi ya wanafunzi waliopo.

Comments