WANAHABARI MBEYA WASHANGAZWA NA HUKUMU

 
Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mbeya (MBPC), Kimeshtushwa na kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mbeya ya kumuachia huru dereva wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta ya Wilayani Chunya, Herman Joseph (33) aliyeshitakiwa kwa kosa la kuwagonga na kuwasababishia ulemavu waandishi wa habari watatu.
Tukio la kugongwa kwa waandishi hao,  Aines Thobias wa kituo cha Clouds Media, Gabriel Kandonga wa ITV, pamoja na mwandishi wa kujitegemea Ibrahim Yasini lilitokea mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka huu katika eneo la Mshewe, Wilayani Mbeya vijijini.
Akieleza kushtushwa na hukumu hiyo, Mwanyekiti wa MBPC,Modestus Nkulu, alisema chama hicho kinatilia shaka mwenendo wa kesi pamoja na hukumu yake iliyotolewa Disemba 13 kwa kuwa haijaleta tija .
Aliongeza kuwa, katika kesi hiyo namba 108/2016  iliyohukumiwa na  hakimu wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Zawadi Laizer , imeibua hisia kali kutokana na mashahidi muhimu ambao ni waandishi wa habari hao waliojeruhiwa kutoitwa mahakamani hapo ili kutoa ushahidi.
“Tangu ajali hiyo ilipotokea Agosti 31, mwaka huu wakati waandishi hao wakielekea kwenye majukumu yao Wilayani Chunya na  kesi kufunguliwa katika kituo cha polisi cha Mbalizi na baadae kupelekwa mahakamani wahusika (majeruhi ambao ni waanmdishi) aliyeitwa kutoa ushahidi” alifafanua Nkulu.
Alisema kitendo cha majeruhi kutoitwa mahakamani kutoa ushahidi kimeleta shaka kubwa dhidi ya hukumu hiyo na kwamba tayari ofisi yake imewasiliana na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ili kupinga hukumu hiyo na kukata rufaa.
 Aidha, Nkulu alisema shaka inaibuka katika maeneo makuu mawili ambayo ni namna ofisi ya upelelezi ilivyoshghulikia suala hilo, pamoja na mwanasheria wa serikali kushindwa kuwapeleka wahanga wa ajali hiyo kutoa ushahidi muhimu.
“Tumeamua kujikita katika maeneo hayo mawili ili kuona tija inapatikana , kwani licha ya michoro kuonesha kosa kuwepo kwa mshitakiwa nay eye kukiri kufanya kosa, lakini hukumu imeshindwa kuleta tija”

Comments