ZAIDI YA MILIONI 72 KUWAKOMBOA WANAWAKE SONGEA

Makao Makuu Ya Manispaa ya Songea


Halmashauri ya Manispaa ya Songea imetoa mkopo wa shilingi milioni 72.5 ambazo ni mapato yake ya ndani katika vikundi vya wanawake na vijana ili kusaidia kujikomboa kiuchumi.

Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema mkopo huo umetolewa mwaka huu kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya sh.milioni 52.5 zilikopeshwa kwa vikundi vya wanawake na vijana.
Amesema kati ya fedha hizo vikundi 73 vya wanawake
vimekopeshwa zaidi ya sh.milioni 36 na vikundi 35 vya vijana vimekopeshwa sh.milioni 16.
Kwa mujibu wa Afisa Habari huyo,katika awamu ya pili Manispaa ya Songea imetoa mkopo wa sh.milioni 20 kwa vikundi,ambapo vikundi vya wanawake 32 vimekopeshwa sh.milioni 15.4 na vikundi 10 vimepewa mkopo wa sh.milioni 4.6.
Amesema vikundi hivyo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika Manispaa hiyo na kwamba mikopo iliyotolewa ni kati ya sh. Laki sita hadi laki nane kwa kila kikundi ambazo zinatakiwa kurejeshwa baada ya miezi 12.
Manispaa ya Songea inatoa riba ya asilimia kumi tu kwa mkopo wa mwaka mmoja ,ambapo asasi nyingi za kifedha zinatoa riba kubwa yenye makato mengi hali inayosababisha wakopaji wadogo kushindwa kufikia malengo yao.
Mkopo huo unatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali vya wanawake na vijana kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1993 ambayo imeagiza kutoa mkopo kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri,lengo likiwa ni kuinua hali ya uchumi katika makundi hayo mawili.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea

Comments