ZAIDI YA WAHITIMU 400 WA UALIMU WA SAYANSI WASHINDWA KUHITIMU KWA KUKOSA ADA YA MUHULA WA MWISHO

Zaidi ya wahitimu 400 waliokuwa wakisomea Shahada ya Ualimu wa Masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Moshi, wameondolewa kwenye orodha ya wahitimu wanaotarajiwa kuagwa Desemba 29, mwaka huu.
Kuondolewa kwa wahitimu hao kunatokana na madai kwamba hawajalipiwa ada ya muhula wa mwisho na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Madai hayo yaliibuliwa jana na wawakilishi wa wahitimu hao, wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo (Mwecauso), Gerald Simon, mbele ya Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (CHADEMA).
"Tatizo ni hiyo ada tu, tumefanya mitihani yetu vizuri na kufuzu, hakuna tatizo jingine. Wahitimu zaidi ya 400 wa kozi ya BEDs waliofanya mitihani ya mwisho Julai, mwaka huu, hawatashiriki mahafali ya tisa yatakayofanyika Alhamisi ya Desemba 29, kwa sababu hawajakamilisha ada," alisema Simon.
Japhet Madenda, mwakilishi wa wahitimu hao, alisema tangazo la kuondolewa kwa majina yao katika orodha ya wahitimu waliliona chuoni hapo Desemba 24, mwaka huu.

Comments