ZAIDI YA WATU 21,000 WANAISHI NA VVU MANISPAA YA SONGEA

Makao Makuu ya Manispaa ya Songea


Zaidi ya watu 21,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wanaishi na virusi vya UKIMWI.
Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema takwimu toka Kitengo cha uratibu wa UKIMWI na tiba katika Manispaa hiyo zinaonesha kati ya watu wenye virusi,watu zaidi ya 10,000 ndiyo wanaugua ugonjwa wa UKIMWI.
Amesema idadi hiyo ya wagonjwa ndiyo wanatumia dawa za kurefusha maisha za ARV na kwamba maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika manispaa ya Songea ni asilimia nne.
Amezitaja kata ambazo zinaongoza kwa maambukizo ya virusi vya UKIMWI katika Manispaa ya Songea kuwa ni Bombambili,Mateka,Ruvuma na Lilambo.
Midelo amesema takwimu za Maambukizi ya virusi vya
UKIMWI(VVU) katika Manispaa ya Songea kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2015 zinaonesha kuwa watu 319 wamegundulika kuwa maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI.
Amesema kati ya waliogundulika wanaume ni 114 na wanawake ni 205 sawa na asilimia 4.2 ya watu waliopima ambao ni 7,510, kati ya hao wanaume 3,417 na wanawake 4,093.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa maambukizo ya virusi katika makundi maalum yamefikia asilimia 36 ambapo kila watu 100 watu 36 wana virusi vya UKIMWI ukilinganisha na kiwango cha kitaifa cha asilimia tano ambayo ni sawa na kila watu 100 watano wana virusi.
Hata hivyo amesema Manispaa imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa janga la UKIMWI linapungua ikiwemo kushirikiana na wadau wa ndani na nje wanofanya shughuli mbalimbali katika Halimashauri ya Manispaa hiyo.
Ameitaja mikakati inayoendelea kufanywa hadi sasa kukabiliana na ugonjwa huo kuwa ni uzuiaji wa maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT), upimaji wa hiari (VTC), upimaji wa kila
mteja anayefika katika vituo vya Huduma (PITC), Huduma ya wagonjwa wenye magonjwa nyemelezi na uanzishwaji wa vikundi vya wenye kuishi na Virusi vya UKIMWI.
Afisa Habari huyo amesema Manispaa ya Songea ina Vituo 24 vya kutolea Huduma ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (CTC) na dawa zinatolewa bila malipo kwa wagonjwa wa Ukimwi .
Amesema Manispaa ina vituo 26 ambavyo hutoa huduma za kuzuia maakumbukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma ya wagonjwa majumbani kwa wenye magonjwa sugu, vituo vimeongezeka kutoka 17 kufikia 20.
Mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa ukiwa na maambukizi ya asilimia saba ambapo Mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza kitaifa ukiwa na asilimia 14.5,nafasi ya pili inashikwa na Mkoa wa Iringa,ikifuatiwa na Mkoa wa Mbeya kwa nafasi ya tatu
na mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya tano.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea

Comments