AMUUA BABA YAKE KWAKUMPIGA NONDO KICHWANI KISHA KUMFICHA STOO
MKAZI wa Kijiji cha Kebeyo Kata ya Mbogi wilayani hapa, Marwa
Nyakogera (28) anatafutwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi
Nyakogera Ramadhan (55) kwa kumpiga na nondo kichwani.
Mtuhumiwa huyo baada ya kuua mzazi wake
alimfungia ndani ya stoo ya nyumba aliyokuwa akihifadhi vyuma chakavu.
Diwani wa Mbogi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kijiji cha Kebeyo, Ezekel
Kebaki na kaka wa marehemu, Werema Chacha, wameeleza hayo kwa nyakati
tofauti.
Kebaki amesema tukio hilo lilitokea kijijini Kebeyo jana usiku
nyumbani kwa Nyakogera (marehemu) wakati alipokuwa akiingia katika stoo,
kukagua vyuma chakavu katika stoo yake anayotunzia vifaa hivyo.
Kebaki alisema Marwa (mtuhumiwa), alikuwa katika stoo hiyo akiwa
amepitia kwenye tundu alilotoboa na kukumbana na baba yake huyo mzazi na
kuanza kumshambulia kwa nondo kichwani na kufa papo hapo.
Alisema baada ya kitendo hicho, mtuhumiwa alifunga mlango kwa nje na kutoroka.
Kaka wa marehemu, Chacha alisema iligundulika kuwa Nyakogera
(marehemu) amekufa baada ya watu kwenda kumuangalia baada ya kutotoka
katika stoo hiyo kwa muda mrefu.
Chacha alisema kulikuwa na mgogoro kati ya mdogo wake (marehemu) na mtoto wake.
Inadaiwa kuwa, Novemba mwaka jana kijana huyo alimwibia baba yake Sh 900,000 za mauzo ya asali kutoka mizinga 200 aliyonayo.
Alisema baba yake alimkamata na kumfungulia kesi ambayo ipo
mahakamani na kijana huyo alidhaminiwa hivyo alikuwa nje kwa dhamana.
"Kumekuwa na vitisho kwa mzazi wake huyo na kwa sasa baada ya tukio
hili la mauaji ya baba, kijana huyo haonekani na anatafutwa kwani
alikuwepo kabla ya mauaji, lakini sasa hivi ametoroka haonekani,
tunasaidiana na wananchi na Polisi kumsaka" amesema Chacha.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema Polisi inamsaka mtuhumiwa.
Aliwaomba wananchi washirikiane na Polisi kuhakikisha anatiwa mbaroni.
Comments
Post a Comment