BAJETI YA ZAIDI YA BILIONI 63 YAPITISHWA MANISPAA YA SONGEA KWA MWAKA WA 2017/2018
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma limepokea,kujadili na kupitisha Bajeti ya mwaka 2017/2018 ya zaidi ya sh.bilioni 63 na milioni 796.
Akiwasilisha bajeti
hiyo Mchumi Mkuu wa Manispaa hiyo Raphael Kimary amebainisha kuwa kati ya fedha
hizo zaidi ya sh.bilioni 16 ni za miradi ya maendeleo ambazo ni ruzuku kutoka
serikali kuu na sh.bilioni 1.785 ni fedha za maendeleo.
Kwa mujibu wa Mchumi
huyo fedha za matumizi ya kawaida ambazo ni ruzuku toka serikali kuu zimetengwa
zaidi ya sh.bilioni 3.893 na matumizi ya kawaida kutoka vyanzo vya ndani zimetengwa
zaidi ya sh. bilioni 1.533.
Amesema mishahara ya
watumishi zimetengwa zaidi ya sh.bilioni 40 na nguvu za wananchi zimetengwa zaidi
ya sh.milioni 175.
Kimary ameliambia
Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo kuwa uandaaji wa Mpango wa Bajeti ya mwaka
huu wa fedha imezingatia Miongozo na maelekezo mbalimbali ya serikali ikiwemo
ukusanyaji wa mapato na utengaji rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
Mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/2017 hadi 2020/2021).
Amebainisha bajeti
hiyo imejikita katika sekta kipaumbele nane ambazo zimepatiwa mafunzo ya
utekelezaji.Amezitaja sekta hizo kuwa ni zilizopo katika Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii,Wazee na Watoto,Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano
na Uchukuzi.
Sekta nyingine
zilizopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni kutoka Wizara ya Kilimo,Mifugo na
Uvuvi, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Wizara ya Fedha na Mipango,Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na
Wizara ya Nishati na Madini.
Amesisitiza bajeti
hiyo pia imezingatia Hotuba ya Rais aliyoitoa katika Bunge la 11,Hotuba ya
Waziri Mkuu ya Januari mwaka huu katika Mkoa wa Ruvuma
ambayo ilikuwa na masuala mtambuka na maelekezo ya viongozi wa Mkoa na Taifa
kwa ujumla.
Comments
Post a Comment