BINTI ALIYEZIKWA KWA SIRI SASA KABURI LAKE KUFUKULIWA
Familia
moja jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike
wa miaka mitatu katika kaburi lililofichwa, huku majirani wakidanganywa
kuwa binti huyo yupo hai.
Taarifa
za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa
kuna mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha
aliyezikwa kwa siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.
Inadaiwa
kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na
ngariba, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake
ikishuhudia.
Kitendo
hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani
Arumeru Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu,
kabla ya mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia
mwaka mpya wa 2017.
Mtendaji
wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa
hizo hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na
ndipo alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi
cha Ngaramtoni.
Kamanda
wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na
kwamba ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye
na hatia, uchunguzwe upya.
“Ndio
kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha
mahakama ili twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli
mtoto huyo amezikwa humo na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza
uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema Kamanda arles Mkumbo.
Baba
wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana
na ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla
ya kupoteza maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo
yanapingana na ripoti ya muuguzi katika duka la dawa lililopo kijiji cha
jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.
“Walimleta mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na kutokwa na damu nyingi,” alidai.
Muuguzi huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo zilipomfikia.
Huku
serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado
kuna familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa,
zinaendeleza mila hiyo kwa siri.
Kwa sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana, kuepuka kukamatwa.
Ngariba
wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe
wasiokuwa na ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo
husababisha uvujaji mwingi wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya
magonjwa mengine.
Comments
Post a Comment