KAYA MASIKINI ZILIZOENGULIWA KIMAKOSA TASAF MANISPAA YA SONGEA ZAANZA KUKATA RUFAA
Kaya masikini 260 kati ya kaya 2692 zilizoenguliwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini katika Manispaa ya Songea zimeandika barua TASAF makao makuu kukata rufaa za kuenguliwa kwao.
Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema kaya 2692
kati ya kaya 7,695 zilizokuwa zinanufaika na ruzuku hiyo zimeenguliwa baada ya
uhakiki wa nyumba kwa nyumba kufanyika mwaka jana,ambapo baada ya uhakiki huo
kaya zenye sifa zimebakia 5003.
Midelo amesema kati ya kaya zilizoenguliwa ilibainika kuwa
kaya 1599 katika Manispaa hiyo sio masikini,kaya 342 walihama katika maeneo
yao,kaya 110 walifariki,kaya 417 zilibainika kuwa ni hewa na kaya 144
hazikuwepo kwenye uhakiki huo.
Hata hivyo amesema Mara baada ya kaya zilizoenguliwa kupata
barua za kuondolewa,yametokeo malalamiko mengi katika kaya hizo hali ambayo
imesababisha Manispaa ya Songea kupita
katika mitaa ya walioenguliwa na kutoa elimu ya kukata rufaa kwa wale
wanaodhani wameonea na wale ambao wametolewa kihalali kuanza kulipa.
Kaimu Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea Mensa Ngerangera
akitoa elimu kwa nyakati tofauti katika mitaa ya Ruhuwiko Kanisani,Ruhuwiko
Shuleni, Namanditi, Lilambo A na Sinai
amewataka wale ambao wametolewa
kwa kukosa sifa waanze kulipa kama ilivyoelekezwa kwenye barua.
Amesema kaya maskini ambazo zimeondolewa kimakosa katika
mpango huo zinatakiwa kukata rufaa kwa kuandika barua TASAF makao makuu na
kwamba ambaye hataandika barua ya rufaa atatakiwa kuanza kulipa deni hilo.
Ngerangera amezitaja sifa za kaya zinazotakiwa kukata rufaa
kuwa ni zile ambazo zinakula mlo mmoja kwa siku,kaya isiwe na zaidi ya heka
moja,asiwe mfanyabiashara,mstaafu wala mwenye mtoto au ndugu wa karibu ambaye
ni mtumishi wa umma na asiwe mwenye nyumba bora iliyoezekwa kwa bati na kupiga sakafu.
Utafiti ambao umefanywa katika baadhi ya mitaa ambayo
wameenguliwa waliokuwa wanufaika, umebaini kuwa kuna kaya ambazo zimeondolewa
kwa makosa kwa kuwa zina sifa ya kaya maskini,ingawa pia zipo kaya ambazo
hazina sifa ya kaya masikini hivyo wanastahili kuenguliwa.
Ngerangera amesema Novemba-Desemba 2016,kiasi cha sh.milioni
277 zimetolewa katika kaya masikini zenye sifa zilizopo katika mitaa 53 ya
Manispaa ya Songea ambapo Januari-Februari 2017 Manispaa hiyo imetoa kiasi cha sh.milioni
256 kwa kaya maskini zenye sifa.
Comments
Post a Comment