MVUA YALETA MAJANGA MAKUBWA HUKO SUMBAWANGA
NYUMBA 160 zimeharibiwa na mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali
zinazoendelea kunyesha wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa huku watu 1,200
wakikadiriwa kuathirika na kukosa makazi ya kudumu.
Nyumba hizo zimeharibiwa na mvua za masika zilizoambatana na upepo
mkali zilizoanza kunyesha katika mkoa wa Rukwa kuanzia Septemba mwaka
jana hadi mapema mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani
Haule, alisema kuwa tathmini ya awali iliyofanyika imebaini kuwa ujenzi
wa chini ya viwango wa nyumba za makazi vijijini ni miongoni mwa sababu
ya nyumba hizo zaidi ya 1,000 kubomolewa kwa mvua za masika na
kuzisababishia familia nyingi hasara kubwa.
Aliitaja sababu nyingine ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana
na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo ukataji na uchamaji miti
ovyo na kusababisha maeneo mengi vijijini yakibaki bila miti ambayo
ingeweza kuzuia upepo mkali.
Alivitaja vijiji vilivyoathiriwa kwa mvua hizo za masika katika
wilaya ya Sumbawanga kuwa ni Uzia kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa
ambapo familia kadhaa zimekosa makazi ya kudumu baada ya nyumba zao 64
kubomolea na mvua hizo. Watu 19 wamejeruhiwa.
Alisema katika tukio hilo nyumba 50 zimeharibika vibaya ambapo paa na
kuta zimeanguka. Vjiji vingine ni Mtimbwa, manispaa ya Sumbawanga
ambapo nyumba 27 ziliharibiwa, mbuzi nane, kuku zaidi ya 100 na nguruwe
mmoja walikufa.
Kijiji cha Mwela katika Bonde la Ziwa Rukwa nyumba 23 ziliharibiwa na
kujeruhi watoto wanne wa familia moja. Katika vijiji vya Mpwapwa na
Jangwani nyumba 43 ziliharibiwa na kumjeruhi mtoto mmoja wa miaka sita
huku zaidi ya watu 250 wakiwa wamekosa makazi ya kudumu.
Comments
Post a Comment