MWALIMU AFUNGWA MIAKA MINNE JELA
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Kagecha iliyopo Kowak, Kata ya
Nyathorogo wilayani Rorya mkoani Mara, Mabogo Wambura (47),
amehukumiwa
kwenda jela miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya
ya madaraka kwa kutoa upendeleo wa zabuni wa ujenzi wa choo.
Amesomewa hukumu hiyo jana katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka
mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Amon Kahimba,
iliyowasilishwa mahakamani hapo na Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mwinyi Yahaya.
Mshitakiwa alikiri kutoa zabuni kwa mshirika wake, Abich Yongo ya
ujenzi wa choo cha shule hiyo iliyogharimu Sh milioni tatu bila kufuata
utaratibu wa kamati za shule hiyo.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Yahaya alidai kuwa mshitakiwa
Wambura akiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kagecha, kati ya Desemba
mosi na 30, mwaka 2014 alitoa zabuni bila kutangaza katika mbao za
matangazo wa ujenzi wa choo cha shule hiyo kilichokuwa kimebomoka na
hakufuata utaratibu hivyo alitumia madaraka vibaya.
Mshitakiwa alikiri kutoa zabuni hiyo bila kufuata utaratibu kama nakala ya mashitaka ilivyodai.
Mwalimu huyo aliiomba mahakama hiyo kumpa adhabu ndogo akidai kuwa na
familia inayomtegemea wakiwemo mke na watoto wanaosoma kwani ndiye
tegemeo la familia yake.
Mwanasheria wa Takukuru alipigilia msumari wa mwisho wa kuiomba
mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
Hakimu Kahimba aliungana na upande wa mashitaka na kumhukumu kwenda
jela miaka minne ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotumia vibaya
madaraka.
Comments
Post a Comment