MWANAFUNZI AFA MAJI AKITOKA KUCHUNGA MIFUGO
MWANAFUNZI wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Maporomoko,
iliyopo katika mji mdogo wa Laela, wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa,
Kelvin Kafwimbi (9),
amekufa maji akijaribu kuvuka Mto Katenza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando akithibitisha tukio hilo. Alisema ni la Januari 8, mwaka huu saa moja jioni usiku katika kitongoji cha Maporomoko kilichopo katika kijiji cha Laela wilayani Sumbawanga.
“Marehemu alivutwa na mkondo mkali wa maji alipokuwa anavuka katika Mto Kanteza ambao ulikuwa umefurika kufuatia mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani. Alikuwa akitokea machungoni ambapo mifugo iliweza kuvuka salama bila tatizo,” alieleza Kamanda.
Kamanda Kyando alisema kuwa uchunguzi wa daktari umeonesha kuwa mtoto huyo alikosa hewa baada ya kunywa maji mengi baada ya kuzama mtoni.
“Mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya maandalizi ya maziko yake," alieleza Kamanda Kyando.
Kyando wamewataka wananchi mkoani humo kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha masika ambapo amewashauri wazazi kuangalia kazi za kuwapa watoto wao na pia kuangalia mazingira ya kufanyia hizo kazi pia mazingira wanayocheza ili kuepukana na vifo vinavyoepukika
Comments
Post a Comment