SONGEA NA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA MANISPAA INAKUWA SAFI MBINU HIZI HAPA



Halmashauri ya Manispaa ya Songea iliyopo katika Mkoa wa Ruvuma imedhamiria kuhakikisha manispaa hiyo inakuwa safi kwa kununua kijiko kimoja ili kurahisisha uzoaji taka.
Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Manispaa imeweka bajeti ya kuhakikisha kifaa hicho kinanunuliwa ili mji wa Songea uendelee kuwa safi muda wote.
Midelo amesema ili kuweka mazingira safi manispaa hiyo
inaendelea kuwahamasisha wananchi kutokiuka kanuni na sheria za afya.
Kulingana na Afisa Habari huyo,Manispaa ya Songea huzalisha taka jumla ya tani 155 kwa siku toka kwenye majengo ya biashara, Taassisi, Viwanda vidogo, Vituo vya kutolea huduma za afya na nyumba za kuishi.
Midelo amesema Halmashauri hiyo ina magari matatu ya kuzolea taka ngumu ambapo magari hayo yana uwezo wa kuzoa tani 94.24 ya lengo la kuzoa tani 124 sawa na asilimia76.
Amesema Manispaa hiyo pia inatarajia kuunda vikundi vya askari wa usafi wa mazingira ambao watasaidia kusimamia usafi katika mitaa yote 95 ya manispaa hiyo.
Midelo amesema mpango wa kuanzisha vikundi hivyo unaendelea vizuri ambapo tayari kata tano kati ya 21 wamewasilisha majina ya vijana walioomba kufanya kazi hiyo.
Amesema Manispaa ya Songea imeamua kutumia vikundi vya askari wa usafi wa mazingira ili kusimamia shughuli za usafi wa mazingira na kuhakikisha hakuna mtu ambaye atachafua mazingira bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema tayari Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo wameunga mkono na kuidhinisha shughuli za usafi wa mazingira ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea zifanywe kwa kutumia vikundi vya askari wa usafi wa mazingira.

Comments