WALIMU WA MASOMO YA SAYANSI BADO CHANGAMOTO SONGEA



Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na upungufu wa walimu 243 wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule za sekondari.
Afisa Habari wa Manispaa hiyo Albano Midelo amesema mahitaji ya walimu wa Sayansi katika Manispaa hiyo ni 375 ambapo walimu waliopo hadi sasa ni 132 tu hivyo kuna upungufu wa walimu 243.
Hata hivyo amesema Manispaa ya Songea ina ziada ya walimu wa 192 wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ambapo mahitaji ya walimu katika masomo hayo ni 536 wakati walimu waliopo ni 728.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika shule za sekondari 24 za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea zina jumla ya walimu 856 wanaofundisha masomo ya sayansi na Sanaa.
Kati ya hao, walimu 503 ni wa kiume na walimu 353 ni wa kike.
Kwa mujibu wa Afisa Habari huyo katika shule za msingi 76 za serikali zenye jumla ya wanafunzi 50,119 wakiwemo wavulana 24,656 na wasichana 25,463 zina upungufu wa walimu 95.
Ameitaja mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo kuwa Halmashauri imeomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutoa kipaumbele kwa Mikoa ya pembezoni kuwapangia Idadi kubwa ya walimu wa sayansi badala ya kupangiwa walimu wa Historia, Kiswahili na Jiografia.

Comments