WANG Yi KUFANYA ZIARA YA KIKAZI TANZANIA
Waziri
wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. WANG Yi anatarajiwa
kufanya ziara ya kikazi nchini tarehe 09 Januari 2017. Mhe. Waziri Wang
Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri na ya kihistoria baina ya
China na Tanzania ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu
kuanzishwa kwake pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano wa
kiuchumi baina ya Tanzania na China.
Wakati
wa ziara hiyo Mhe. Wang Yi atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa lengo la kumsalimia.
Aidha,
Mhe. Wang Yi atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Mahiga kuhusu
masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na China na
ushirikiano wa kimataifa.
Itakumbukwa
kwamba, Desemba 2015 kweneye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na
China, China iliichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nne Barani
Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua kwenye maendeleo ya viwanda.
Kupitia mpango huo inatarajiwa viwanda takriban 200 vitajengwa au
kuwekezwa nchini kutoka China kabla ya mwaka 2020.
Mpango
huu unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2020
na pia ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John
Pombe Joseph Magufuli wa kujenga Tanzania ya viwanda. Ni matarajio yetu
kuwa, Watanzania takriban laki mbili watanufaika na ajira kupitia mpango
huu mahsusi wa kuendeleza viwanda.
Mbali
na mpango wa uendelezaji wa viwanda, viongozi hawa wawili watazungumzia
miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi kuisadia Tanzania
ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya Reli ya TAZARA; Ujenzi wa
Bandari ya Bagamoyo pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati.
Aidha,
Mhe. Wang anatarajiwa kuzungumza na Mwenyeji wake kuhusu masuala ya
ushirikiano wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mageuzi ya Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa ambapo China inaunga mkono msimamo wa Afrika na wa
Tanzania wa kutaka Afrika ipewe viti viwili vya kudumu kwenye Baraza
hilo na kura ya turufu.
Vilevile
viongozi hao watazungumzia masuala ya amani na usalama katika eneo la
Afrika Mashariki pamoja na eneo la Bahari ya Kusini mwa China.
Mazungumzo
hayo yatafuatiwa na Mkutano wa Mawaziri na Vyombo vya Habari (Joint
Press Conference) ambapo wataeleza makubaliano waliyofikia kwenye
mazungumzo yao.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
05 Januari, 2017
Comments
Post a Comment