WATANZANIA WATAHADHARISHWA KUHUSU MAFUA YA NDEGE
Ummy Mwalimu |
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewatahadharisha
Watanzania juu ya kuwapo kwa virusi vya ugonjwa wa mafua ya ndege.
Ugonjwa
huo umegundulika kuwapo katika nchi jirani ya Uganda ambako taarifa
zinaeleza kuwa maeneo yaliyoathirika ni yale yanayozunguka Ziwa
Victoria.
Tahadhari
hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia taarifa
yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano
Serikalini- Afya.
“Ugonjwa
huu umegundulika baada ya kuwapo kwa vifo vingi vya ndege pori katika
maeneo ya Lutembe Beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata nchini
Uganda.
“Vilevile,
vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na
inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa
ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya,” alisema.
Waziri Ummy alisema vifo hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu Januari 2, mwaka huu na vimeonekana kuendelea hadi sasa.
“Kwa hapa nchini hakuna vifo vya ndege vilivyoripotiwa hadi sasa,” alisisitiza.
Alisema
ingawa hadi sasa hakuna binadamu aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa
huo nchini Uganda, tahadhari inatolewa kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa
wa kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga
hazitazingatiwa.
Waziri Ummy alisema ugonjwa huo unasababishwa na virusi aina ya Influenza na huenezwa na ndege pori wanaohama hama.
Alisema ndege hao hubeba virusi vya ugonjwa huu bila ya kuonesha dalili za ugonjwa.
“Hivyo
huweza kuambukiza ndege wanaofugwa majumbani mfano kuku na bata wakati
wanapokutana nao. Aidha ndege hao huweza kuambukiza ugonjwa kupitia njia
ya kinyesi ambacho hudondoshwa ardhini au kwenye mabwawa na madimbwi ya
maji,” alisema.
Aliongeza: “Kwa
kuwa binadamu huwezaa kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au
kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu. Ni muhimu kutokugusa
mizoga ya ndege pori au kinyesi chake.”
Alisema
kuwa binadamu anaweza pia kupata maambukizi wakati wa kuchinja kuku,
kunyonyoa manyoya, na wakati wa kutayarisha kabla ya kumpika.
Waziri
Ummy aliwataka wananchi watoe taarifa iwapo wataona dalili zozote za
ugonjwa na vifo katika jamii ya ndege wa kufugwa na ndege pori.
“Kuna
uwezekano wa virusi hivi kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye
uambukizo kwenda kwa binadamu mwingine, na hii ikitokea inaweza
kusababisha mlipuko mkubwa unaoweza kusambaa pande zote za dunia,” alisema.
Comments
Post a Comment