WATU WAZIMA ZAIDI YA 3,400 MANISPAA YA SONGEA WANA TATIZO LA KKK

Afisa Habari Wa Manispaa Ya Songea Albano Midelo


Jumla ya watu wazima 3,460 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma hawajui Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.



Hayo yameelezwa na afisa Habari wa Manispaa ya Songea Albano Midelo ambapo amesema kati ya watu hao,wanaume ni 1,720 na wanawake ni 1,740 ambapo  takwimu za idadi ya watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 19 hadi 65 katika Manispaa hiyo ni 180,240 kati yao wanaume ni 88,093 na wanawake 92,149.



Hata hivyo amesema elimu ya watu wazima katika Manispaa ya Songea inatekelezwa katika miradi mbalimbali ambayo ni  Lanes, MUKEJA, KCM,KCK,Ndiyo Ninaweza na Ufundi na kwamba Manispaa ina  idadi ya vikundi 64  vyenye washiriki 3,333 wakiwemo wanaume 1,493 na wanawake 1,840.



Licha ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa elimu ya watu wazima nchini,Afisa Habari huyo ametaja mafanikio ambayo yamepatikana katika elimu ya watu wazima katika Manispaa hiyo kuwa ni udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza umepanda toka  asilimia 84.6 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 98.5 mwaka 2016.



Amesema hali hiyo kutokana na utekelezaji wa Elimu bila Malipo,kupanda kwa ufaulu katika mitihani ya kidato cha Nne na Sita na uanzishwaji wa shule ya sekondari Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya Kidato cha Tano na Sita.



Mafanikio mengine ni Ujenzi  wa Hosteli ya wasichana katika sekondari ya Matogoro na kumaliza tatizo la meza na viti katika shule za sekondari katika Manispaa ya Songea.



Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2002,kulikuwa na  watu wazima milioni 5.5  katika nchi nzima sawa na asilimia 32 ya watu ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Idadi ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika imeendelea kuongezeka na kufikia zaidi ya watu milioni 10 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.


Comments