ZITTO KABWE ASEMA WATANZANIA WAKIFA NJAA TUTAIWAJIBISHA SERIKALI
Mbunge
wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema endapo Mtanzania yeyote atakufa
kwa njaa watachukua jukumu la kumwajibisha Rais kwa kusema waziwazi
kwamba hajatimiza wajibu wake.
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Kijichi jana, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto alisema, “Tunamkumbusha
Rais kwamba kwa mujibu wa ibara ya 46A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, ambayo yeye amekula kiapo kuilinda, kuihifadhi na
kuitetea, Bunge laweza kumshtaki kwa kosa la mwenendo unaodhalilisha
kiti cha Rais. "
Kauli
hiyo ya Zitto ilitokana na msimamo wa Rais Magufuli kuwa hakuna njaa
nchini na kwamba Serikali haitatoa chakula cha msaada, huku makundi
mengine ya wananchi, wakiwamo wanasiasa na viongozi wa dini wakisema
kuna upungufu wa chakula uliotokana na ukame.
Zitto ambaye kabla ya kuhutubia alipita nyumba za jirani na uwanja akisalimia, alisema, “Tumesema
hili la njaa katika kutekeleza wajibu wetu, Rais na Serikali wamejibu
na kufunga mjadala. Wakati utaamua na kuonyesha mkweli nani na mpiga
propaganda nani.”
“Tunamwambia
Rais kwamba, Mtanzania yeyote akifa kwa njaa kwa sababu Serikali
imeshindwa kutekeleza wajibu wake, Watanzania tutapaswa kuchukua hatua,
Katiba inatulazimisha kumtoa Rais madarakani.
“Jambo
moja ni muhimu sana, Rais anapaswa kujua kuwa anafanya kazi kwa mujibu
wa Katiba ya nchi. Na Katiba imetoa wajibu wa lazima kwa Serikali
kulinda watu. Ndio kazi ya Serikali – kulinda wananchi pale ambapo
yanatokea majanga ambayo yanazidi kimo wananchi hao,” aliongeza.
Alisema
Rais yupo chini ya Katiba na kwa idadi ya wabunge wa upinzani waliopo
bungeni, na wakiamua kusimama na wananchi kulinda Katiba, anaweza kuwa
wa kwanza wa nchi yetu kutolewa hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni.
“Katiba inahitaji asilimia 20 tu ya wabunge kuwasilisha hoja hiyo bungeni,” alisema.
Mbunge
huyo alitoa wito kwa Watanzania bila kujali vyama vyao, kuweka rekodi
ya hali ya chakula popote walipo na kuweka takwimu ya maafa yeyote
yanayotokana na njaa.
Alimtaka
Rais atumie lugha ya kujenga matumaini badala ya kujenga hofu kwenye
jamii, aache kuonea watu kwa kutumia madaraka yake, na akumbuke cheo ni
dhamana.
Kiongozi
huyo alisema ameamua kusema hayo kwa sababu baada ya siku saba
hawatakuwa na nafasi ya kuzungumza majukwaani kama viongozi wa vyama vya
siasa kwa sababu ya zuio lisilo la kikatiba la kuzuia mikutano ya
hadhara.
Hata hivyo, sheria inasema janga la njaa linaweza kutangazwa na Rais tu na si mtu mwingine.
Comments
Post a Comment