AFISA MTENDAJI APANDISHWA KIZIMBANI KWAKUOMBA NA KUPOKEA RUSHWA YA SH. 10,000
OFISA Mtendaji wa kijiji cha Panyakoo, wilayani Rorya, mkoani Mara, Elenthan Milton (34), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime kwa mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh 10,000.
Imedaiwa mahakamani kuwa rushwa hiyo ameipokea kutoka kwa mkazi wa kijiji hicho, Amos Willson.
Mwananchi huyo alihitaji kuandikiwa barua na mtendaji huyo ya kwenda kumdhamini ndugu yake aliyekuwa na kesi mahakamani.
Amesomewa mashitaka katika kesi namba 111/2017 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Marther Mpaze.
Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Mwinyi Yahaya, amedai kuwa mshitakiwa Milton akiwa ofisa mtendaji wa
kijiji cha Panyakoo, wilayani Rorya, Julai 11 mwaka jana akiwa ofisini
kwake, alimuomba Willson Sh 10,000 ili amwandikie barua ya kwenda
kumdhamini ndugu yake aliyekuwa na kesi mahakamani.
Yahaya amedai Willson hakuwa na fedha hizo wakati huo na kuahidi
kuifuata nyumbani na ndipo alipofika Ofisi za Takukuru, kutoa taarifa na
kuongozana na maofisa wa taasisi hiyo kwenda kumpa Milton fedha hizo na
ndipo alipokamatwa.
Mshitakiwa amekana mashitaka na amepelekwa rumande baada ya wadhamini kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.
Kesi hiyo itatajwa tena Machi 7 mwaka huu.
Comments
Post a Comment