MMOJA AFARIKI DUNIA KWA KIPINDUPINDU HUKO KIGAMBONI


Image result for kipindupindu




















MKUU wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Hashimu Mgandilwa amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanaweka mazingira safi kuondoa hatari ya kukumbwa na kipindupindu.
Amesema, ugonjwa huo umekumba kaya mbili katika wilaya hiyo,
mtu amefariki dunia na wengine kadhaa wameugua na tayari wameudhibiti.
Mgandilwa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya ugonjwa huo katika wilaya hiyo baada ya kudaiwa kuwepo kwa wagonjwa.
Amesema, watu 15 wa familia mbili walibainika kuwa na kipindupindu baada ya mmoja wao kufariki dunia kwa ugonjwa huo.
“Watu hawa walibainika kuwa na ugonjwa huo wiki iliyopita baada ya mmoja wa familia hiyo kurejea kutoka msibani Rufiji na kuanza kulalamika maumivu ya tumbo wakiwa njiani kumpeleka hospitali alifariki na wao waliamua kumzika kienyeji hali iliyosababisha ugonjwa huo kusambaa hata kwa wale ambao hawakutoka Rufiji,” alisema Mgandilwa.
Amesema baada ya kufariki dunia kwa mtu huyo walifanya juhudi za kuwapeleka Hospitali wengine ambapo 11 kati ya 15 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine wanne bado wanaendelea na matibabu.
“Kwa kweli tumejitahidi sana kudhibiti ugonjwa huu, tusingekuwa makini leo tungeweza kuwa na wagonjwa zaidi ya hamsini lakini tunaweza kusema tumeweza kudhibiti,” alisema.
Amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha wanakunywa maji yaliyochemshwa na kuhakikisha wanapasha vyakula vilivyokaa muda mrefu pamoja na kunawa mikono kabla na baada ya kula.
Aliongeza kuwa maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Kibada Tungi na Kisarawe hivyo ili kudhibiti ugonjwa huo watapiga dawa maeneo hatarishi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi.

Comments