SHAMRA SHAMRA ZA MIAKA 40 YA CCM KUFANYIKA KITOFAUTI MWAKA HUU
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefuta sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya
chama hicho zilizokuwa zifanyike kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amewataka wanachama wote nchini
kuadhimisha siku hiyo kwa kushiriki kwenye shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi
wa madarasa, wodi za wagonjwa kwenye zahanati na vituo vya afya, kufanya usafi
na kuwatembelea wagonjwa hospitalini.
“Pia tunawataka viongozi na wanachama wa CCM ngazi za mikoa, wilaya, jimbo,
kata na mashina kuwa na mikutano ya ndani itakayotoa fursa kwa uhuru na uwazi
kujadili tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Wajadili changamoto,
matatizo waliyonayo, wakosoe, wakosoane na kutoa mbadala,” amesema Polepole.
Ameongeza kuwa mikutano hiyo ya ndani itawasaidia wanachama kuwa na uelewa
wa pamoja juu ya changamoto na matatizo waliyonayo na mambo mazuri ya kujivunia
kama chama kwa miaka 40 lakini pia itawawezesha kutoka na mwongozo wa chama wa
mwaka 2017.
Comments
Post a Comment