TAA YAWAKA MASHINDANO YA BALOZI WA UTALII RUVUMA

Mratibu wa Kituo cha Habari za Utalii Mkoa wa Ruvuma Samson Kahabuka


Mashindano ya kumtafuta Balozi wa Utalii wa Mkoa wa Ruvuma ambayo yanaratibiwa na Kituo cha Habari wa Utalii cha Mkoa wa Ruvuma yameanza kwenye Hoteli ya Majimaji mjini Songea.



Mratibu wa Kituo cha Habari za Utalii katika Mkoa wa Ruvuma Samson Kahabuka amesema warembo 15 kutoka Wilaya ya Songea wameanza mazoezi kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Majimaji ambapo lengo ni kupata warembo kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma.



Kahabuka amelitaja lengo la shindano hilo ni kutangaza vivutio vyote vya Mkoa wa Ruvuma,ambapo Februari10,warembo15 kutoka Wilaya ya Songea watambelea Wilaya ya Nyasa ili kuona baadhi ya vivutio vya wilaya hiyo.



“Warembo hao watakuwa Nyasa kwa siku mbili,wataona vivutio na kufanya tamasha usiku kwenye Ukumbi wa Bay Live ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa’’,alisemaKahabuka.



Hata hivyo amesema Februari 13,watapokelewa warembo kutoka wilaya nyingine,ili kuanza mazoezi rasmi ya kumsaka Balozi wa utalii yakishirikisha wilaya za Songea, Nyasa,Namtumbo,Tunduru na Mbinga yataanza kwenye hoteli ya Majimaji.



Amesema kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Februari hadi Machi,warembo hao watafanya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii ambavyo vipo katika Mkoa wa Ruvuma.



Mratibu huyo amesema fainali za kumpata Balozi wa utalii Mkoa wa Ruvuma zinatarajiwa kufanyika Machi 31,2017 mjini Songea.



Ameyataja baadhi ya manufaa ambayo mshiriki atayapata katika shindano hilo ni kupata elimu ya mambo mtambuka ikiwemo elimu ya kujitambua,fursa ya ajira kwenye hoteli na atakayeshinda atawakilisha Mkoa wa Ruvuma ngazi ya kitaifa.

Comments