WABUNGE WALILIA FEDHA ZA BAJETI, WATAKA ZIFIKE HARAKA MAENEO HUSIKA



Wabunge wameicharukia Serikali kwa kutofikia lengo la kupeleka fedha za maendeleo katika robo ya kwanza ya bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo inaonyesha  taasisi nne ziko katika hali mbaya kwa kutopelekewa kabisa.

Taasisi hizo zimetajwa kuwa ni Ofisi ya Bunge, Tume ya Umwagiliaji, Idara ya Mifugo na Zimamoto na Uokoaji.

Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti ya kipindi cha  Januari 2016 hadi Januari 2017, iliyosomwa bungeni jana na mwenyekiti wake, Josephat Kandege, ilisema Mamlaka ya Serikali za Mitaa nayo imo katika kundi la walioathirika kwa kupata fedha kwa asilimia 57.

Kandege alisema kamati ilibaini mbali na Serikali kuvuka lengo la kupeleka fedha za matumizi ya kawaida (OC) lakini haikupeleka fedha yoyote kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za utawala kwa halmashauri zote nchini.

“Pia, Serikali ilipeleka asilimia 19 tu ya fedha za matumizi ya kawaida zilizotengwa kwa ajili ya kugharimia sekta ya afya. Hali hii imesababishwa na baadhi ya mafungu kupewa fedha nyingi zaidi ya zilizokuwa zimepangwa kutolewa katika kipindi husika,” alisema.

Comments