WATU 585 WAMEUAWA MKOANI TABORA KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2015/2016



Watu 585 wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mkoani Tabora kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za wivu wa mapenzi, ulipizaji kisasi, imani
za kishirikina na ujambazi.

Kwa takwimu hizo, takriban watu 24 huuawa kila mwezi mkoani humo.

Akizungumza wakati wa mafunzo elekezi kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa alisema mwaka 2015 waliuawa watu 310 na wengine 275 mwaka 2016.

Alisema mbali na matukio ya mauaji kupungua kwa watu 35, bado idadi ya mauaji ni kubwa mkoani Tabora; huku Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ikiongoza kwa kupoteza watu 84 mwaka 2015 na 75 mwaka jana.

Alitoa mfano wa mume na mke waliouawa kwa kukatwa mapanga Januari. Alisema polisi waliwakamata vijana wawili wakidaiwa kutekeleza mauaji hayo ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya kuahidiwa kulipwa Sh6.3 milioni na walilipwa Sh1.6 milioni zikiwa ni malipo ya awali.

Alisema vijana hao kutoka wilayani Kaliua walikamatwa wakisubiri malipo ya mwisho.

Kamanda Issa alitoa mfano mwingine wa kijana aliyekodiwa kuua ili kulipiza kisasi lakini alikosea na kumuua mtu mwingine.

Issa alisema kijana huyo alikamatwa baada ya kutokea mabishano kuhusu malipo na aliyemtuma kufanya mauaji hayo.

Kaimu Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Urambo, Maarifa Akanga alisema kuna uhusiano kati ya watu kutoka nje na mauaji hayo, hivyo Kaliua kuwa na idadi kubwa ya matukio hayo. Alisema baadhi ya watu hutekeleza matukio ya mauaji kwa malipo ya Sh400,000.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliwataka wananchi kuacha mauaji ambayo mbali ya kuwa ni kosa la jinai, pia ni kinyume na maagizo ya Mungu.


Comments