AKAUNTI ZA CUF ZAPIGWA KUFURI NA MAALIM, LIPUMBA ALALAMIKA

Profesa Ibrahimu Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad
Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba amelalamikia kitendo cha Katibu Mkuu wa chama hicho,
Maalim Seif Sharrif Hamad kuzifunga  akaunti zote za chama hicho za wilaya.

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha baraza la uongozi linaloongozwa na upande wake. Profesa Lipumba amesema kutokana na uamuzi huo ruzuku ya chama kutoka serikalini wameikosa.

“Wajumbe nawashukuru kwa kuja ili kupata fursa ya kujenga chama. Chama chetu kipo ndani ya mtihani ambao kwa kweli chanzo chake ni Katibu Mkuu wetu kutoheshimu katiba yetu na kutoheshimu taratibu za kidemokrasia,” amesema Prof. Lipumba.

Aidha, Prof. Lipumba amesema kuwa Maalim Seif alitakiwa kuhudhuria kikao hicho na alipewa taarifa lakini hakuweza kufika, hali iliyosababisha majukumu yake kusimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara. Magdalena Sakaaya.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Mazrui amesema kuwa hatua ya kufunga akaunti za benki imelenga kulinda fedha ya chama ili zisitumiwe vibaya na upande wa Profesa Lipumba.
Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa bado anamtambua Prof. Lipumba kuwa ni Mwenyekiti wa chama hicho kwa kuwa hakuwa na taarifa kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu.

Comments