AUDIO: RC RUVUMA AAGIZA SONGEA KUJENGA DAMPO LA KISASA

Endelea kutembelea blog yetu kuwa wa kwanza kuhabarika kwa maoni na ushauri +255 766 086 039 +255 625 715 167 +255 744 063 802 +255 719 980 891 +255 684 219 786
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk. Binilith Satano Mahenge (Aliyesimama)
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk.Binilith Mahenge amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea,Tina Sekambo kuwalipa fidia ya sh.milioni 22 wakazi wa Subira ambako Manispaa ya Songea imechukua eneo la ekari 25 kwa ajili ya ujenzi wa dampo la kisasa la kutupia taka.


Akizungumza na watumishi wote wa Manispaa hiyo kwenye ukumbi wa Manispaa hiyo katika ziara yake ya siku moja ya kukagua maghuba ya taka,Dk.Mahenge amesema wakati Manispaa inafanya utaratibu wa kujenga dampo hilo,hivi sasa litafutwe eneo maalum nje ya Mji kwa ajili ya kumwaga taka zinazozalishwa katika Manispaa hiyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Abdul Hassani Mshaweji amemuakikishia Mkuu wa Mkoa kutekeleza agizo hilo ambapo amesema, Manispaa ina maeneo mawili nje ya mji ambayo yanaweza kutumika kwa muda kutupa taka wakati maandalizi ya ujenzi wa dampo la kisasa unafanyika.
Awali akisoma taarifa ya Manispaa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Tina Sekambo amesema Manispaa inazalisha taka kiasi cha tani 71.5 kwa siku ambapo uwezo wa Manispaa hiyo kuzoa taka kwa siku ni kati ya tani 35 hadi 40 hali inayosababisha tani 31.5 kubaki bila kuzolewa.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema tangu Januari mwaka huu Manispaa hiyo haina sehemu maalum ya kutupa taka kutokana na wananchi wa Mwengemshindo ambako taka zilikuwa zinatupwa Kuzuia magari yasimwage tena taka.
Kwa upande wake Afisa Usafi na Mazingira wa Manispaa ya Songea,Philipo Beno amesema Manispaa ina jumla ya Maghuba 33 ambapo baadhi ya maghuba yamebainika kuchangia uchafu wa mji.
Ameyataja maghuba hayo kuwa ni Mangolingoli,sovi, Mchele na Mamboleo ambapo uongozi wa Manispaa unafikiria kuyafuta Maghuba hayo ili kuboresha usafi wa mji.
“Idara inatarajia hivi karibuni kupokea kijiko (Mtambo wa kuzolea taka) hivyo kitarahisisha ukusanyaji wa taka na kupunguza muda wa kuzoa taka kwa kutumia nguvu kazi’’,anasisitiza Beno.
Hata hivyo Beno amesema Idara yake, imeanza kuyaondoa Maghuba yaayochafua hali ya mji,ambapo hadi sasa limeshaondolewa ghuba la stendi ya Bombambili na kwamba Idara ina mpango wa kugeuza taka kuwa fursa kwa kutumia vikundi vya usafi wa mazingira.
Manispaa ya Songea ndiyo kioo cha Mkoa wa Ruvuma, ina Kata 21,Mitaa 95 ikiwa na jumla ya watu 218,942 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
Mei 29,2017

Ingia kwenye link hizo hapo chini kuwasikiliza mkuu wa mkoa na afisa mazingira ⇓
https://www.audiomack.com/song/ukweli-100/mkuu-wa-mkoa-wa-ruvuma
https://www.audiomack.com/song/ukweli-100/afisa-mazingira 

Comments