CWT YAMWAGA VIFAA VYA MICHEZO MANISPAA YA SONGEA

Endelea kutembelea blog yetu kuwa wa kwanza kuhabarika kwa maoni na ushauri +255 766 086 039 +255 625 715 167 +255 744 063 802 +255 719 980 891 +255 684 219




Chama Cha Walimu(CWT) katika Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma kimetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh.360,000 ili timu za Manispaa hiyo zinazojiandaa kwa michezo ya UMITASHUMTA Mkoa wa Ruvuma.

Mwenyekiti wa CWT katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mathias Mwanjisi akizungumza wakati anakabidhi vifaa na fedha hizo kwa Afisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo Edith Kagomba amesema CWT imetoa mipira minne ambayo itasaidia timu za Manispaa kufanikisha michezo ya mwaka huu.

Mwanjisi amesema kila mpira una thamani ya sh.60,000 na kwamba mipira iliyotolewa ni kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu(football),mpira wa wavu(volleyball),mpira wa pete(netball) na mpira wa mikono(handball).

“CWT ilipokea barua ya kuomba msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo kwa ajili ya UMITASHUMTA kutoka Idara ya Elimu Msingi ili  kuunga mkono juhudi za serikali za kuendeleza michezo tumeamua kutoa msaada huu wa vifaa vya michezo’’,alisema Mwanjisi.

Kwa upande wake Katibu cha CWT katika Manispaa ya Songea Esther Chaburuma amesema katika kuhakikisha wachezaji katika Manispaa hiyo wanafanya vizuri katika michezo ya UMITASHUMTA,CWT pia imetoa fedha taslimu kiasi cha sh.100,000 kwa ajili ya kununulia jezi za wachezaji.

Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Songea Edith Kagomba amekishukuru CWT kwa msaada wa vifaa hivyo vya michezo ambavyo amesema vitasaidia wachezaji wa Manispaa hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya UMITASHUMTA mwaka huu.

Naye Afisa Michezo wa Manispaa ya Songea Andrew Mwafalo amesema maandalizi ya  kuweka kambi ya UMITASHUMTA katika ngazi ya shule,kata na tarafa ambayo yalianza mwanzoni mwa Mei yamekamilika ambapo tayari timu zimeingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa wa Ruvuma ambayo yanatarajia kuanza  Juni tisa mwaka huu.

Mwafalo amesema Manispaa ya Songea katika michezo ya mwaka huu inatoa timu katika mpira miguu,pete,mpira wa mikono,riadha na timu kwa wenye ulemavu.

UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa wa Ruvuma inatarajiwa kushirikisha Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Namtumbo,Mbinga Mji,Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Tunduru,Nyasa na Madaba.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
Mei 26,2017
Zaidi ingia kwenye link hapo chini kusikiliza
 https://www.audiomack.com/song/ukweli-100/mwenyekiti-cwt

Comments