MADEREVA BAJAJI MBEYA WASITISHA KULIPA USHURU WAKIDAI HAKI ZAO

Endelea kutembelea blog yetu kuwa wa kwanza kuhabarika kwa maoni na ushauri +255 766 086 039 +255 625 715 167 +255 744 063 802 +255 719 980 891 +255 684 219 786

Mwenyekiti wa chama cha wamiliki na madereva bajaji jijini Mbeya Idd Ramadhani

Madereva bajaji jijini Mbeya wamegoma kulipa ushuru kwa kile wanachodai kuwa askari wa jeshi la polisi mkoani hapa kuwanyanyasa na hivyo kusababisha wao kushindwa kufikia malengo wanayokusudia kwa siku.


Wakizungumza kwa hisia baadhi ya madereva hao wamesema wamekuwa wakizuiwa kuingia kwenye baadhi ya maeneo kupakia abiria huku jeshi la polisi likitumia nguvu zaidi katika kukabiliana na madereva hao hali inayohatarisha usalama wao.

Mmoja wa viongozi wa madereva hao Angetile Mwalusambo amesema wamekuwa wakinyanyaswa na jeshi la askari polisi kwa kupigwa, kuharibiwa bajaji zao bila sababu za msingi huku maeneo kama barabara kuu, maeneo ya masoko wakiwa hawatakiwi kuchukua abiria wala kukatisha.


Amesema kwa jijini Mbeya ni bora ukauza madawa ya kulevya au kusafirisha wahamiaji haramu kuliko kufanya biashara ya bajaji jambo ambalo limesababisha kujenga uadui baina ya polisi na madereva bajaji.
Pia ameeleza ugumu wanaoupata katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kwa pamoja wameazimia kutolipa ushuru kwa kuwa wanaona hakuna umuhimu wa kulipa ushuru ikiwa hawajatengenezewa mazingira rafiki ya kufanyia kazi.

Ameongeza kwa kusema kuwa wanamshukuru rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete kuwawezesha kupata ajira na wamekuwa wakilipia kila kitu kwenye vyombo vyao lakini bado manyanyaso kutoka kwa askari wa jeshi la polisi.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chama cha wamiliki na madereva bajaji jijini Mbeya Dickson Kiswaga amesema masharti ambayo wamepewa ni magumu hivyo kufanya kazi imekuwa ngumu kwao huku jeshi la polisi likitumia nguvu zaidi na kupelekea madereva kuwachukia na kujenga uadui mkubwa.
Pia ameiomba serikali kuliangalia upya suala la bajaji kutumia barabara kuu huku akilitaka jeshi la polisi kutumia ustaarabu wakati wa kuwakamata madereva bajaji kwa kuwa wao sio majambazi wanafanya kazi halali na hawavunji sheria.

Naye mwenyekiti wa chama cha wamiliki na madereva bajaji jijini Mbeya Idd Ramadhani amethibitisha kufanyika kwa mgomo huo huku akisema wao wamekubaliana na hatua ya madereva hao.

Madereva hao wamesema hawatalipa ushuru hadi hapo manyanyaso hayo yatakapomalizika na kuruhusiwa kufanya kazi maeneo ambayo wamezuiliwa na askari watakapoacha kutumia nguvu dhidi yao.

Comments